NEW

6/recent/ticker-posts

Advertisement

​Hekima za Askofu Bagonza leo:


ROYAL TOUR NI WAZO ZURI LAKINI....

Nimetafakari sana kabla sijaandika maneno haya. Nina wazo gumu na mkono wangu hauna uwezo wa kuandika wazo langu kwa usahihi. Huu ni ulemavu wa wengi. Unachokitaka unakijua lakini kukiandika kwa usahihi huwezi. 

Huku vijijini ukipata mgeni wa kulala, unamwandalia chumba. Wakati mwingine chumba cha kulala ndiyo stoo. Unachukua mashuka na vitenge unafunika visivyohusika. Mgeni analala na baadaye anaondoka bila kujua vilivyofunikwa na vitenge. Anafurahia ukarimu na kuahidi kurudi. Mgeni akikaa sana, kuna hatari ya kujua yaliyofunikwa.

Royal Tour ya Mama ni wazo zuri. Siku hizi kibaya na kizuri vyote vinajitembeza. Usipojitembeza utadoda.

Lakini Royal Tour inahitaji usuluhishi na mambo yetu ya chumbani yaliyofunikwa kwa vitenge. Wageni wakija wakayafunua, TUTAAIBIKA. Tumefunika haya:

1. Uhuru wa habari HAKUNA. Mama ananadi nchi, huku nyuma Msigwa anafungia magazeti. Watalii hushamiri penye uhuru wa habari. Serikali iache kuwa mhariri wa magazeti, redio na televisheni. Atakayekashifiwa aende mahakamani. Taifa lenye mtazamo mmoja si kivutio cha watalii.

2. Uhuru wa Kisiasa HAKUNA. Hata chama tawala hakiko huru kufanya siasa. Bila uhuru wa kisiasa Taifa linageuka kuwa TALIBAN STATE. Mtutu wa bunduki una thamani kuliko katiba na mahakama.

3. Haki za Binadamu HAKUNA. Bila haki za Binadamu, wanawake si sawa na wanaume, weusi si sawa na weupe na matajiri si sawa na Maskini. Tumeona watu wanahoji HANGAYA kuwa Chifu kwa sababu tu, hana ndevu! Bila haki za Binadamu, ROYAL TOUR ni pipa lililotoboka. Halihifadhi maji.

4. Usawa mbele ya sheria HAKUNA. Matokeo yake, wenye madaraka wana haki zaidi mbele ya sheria kuliko wasio na madaraka. Hili ni tanuru la machafuko kwa sababu kuna wanaoamini haki iko mikononi mwao. Tunaishi kwa utulivu si kwa amani.

5. Uhalali (legitimacy) HAKUNA. Kukubalika hutokana na uhalali. Tuna mfumo wa utawala unaopungukiwa na uhalali. Ulipita bila kupingwa, ulipigiwa kura bila kuchaguliwa, ulichaguliwa bila kukubaliwa na uliapishwa bila kuhalalishwa. Hili ni deni la dhamiri. Halilipiki kibinadamu. Mungu tu ndiye Pay Master. Inatisha kukutana naye mubashara. Katiba Mpya yaweza kupunguza kero hii.

Haya 5 na mengine madogo madogo ni mazito kuliko Royal Tour. Tuchague kati ya kupata wageni watakaokuja na kuahidi kurudi tena na wale watakaokuja na kuapa kutorudi tena.

Tukisafisha nyumbani, watakuja na kuahidi kurudi tena. Tusiposafisha, hata wenyeji wataondoka. Dhuluma haivumiliki.

Post a Comment

0 Comments