Wanaume wote ni wale wale. Hii ni miongoni mwa kauli ambazo zimeshika kasi sana katika jamii ikimaanisha kuwa wanaume wote wanafanana. Ijapokuwa kuwa kwa sehemu fulani naweza kukubaliana na kauli hii kwa msingi fulani lakini bado kuna kuna uhalisi ambao ni zaidi ya ukweli huu. Hapa kuna ukweli na kuna uhalisia. Ukweli ni kuwa wanaume wanafanana kwa kiasi kikubwa lakini ukiangalia kwenye uhalisi utagundua kuwa hata katika kufanana kwao kuna tofauti fulani fulani miongoni mwao. Nilipoandika kitabu cha Usichojua Kuhusu Wanaume, niliangazia zaidi mambo yanayowaleta pamoja wanaume. Zile tabia ambazo utaziona angalau kwa kila mwanaume. Hata hivyo kuna vitu ambavyo vinaweka utofauti baina ya mmoja na mwingine bila kuondoa vile vinavyowafananisha. Kuna wale ambao walifanikiwa kusoma kitabu change na wakapata majibu ya maswali yao na kumudu kuishi kwa furaha na wenzi wao na kuna wale ambao bado walishindwa kuelewa maana ni kama kulikuwa na mambo ambayo yalikuwa nje na wigo wa kitabu kile. Je, hii ni kusema kuwa wanaume wapo tofauti? La hashaa
Ila tu kuna vitu na mambo ya ziada unaweza kuyaona kwa mwanaume mmoja usiyaone kwa mwingine. Na andiko hili ni katika jitihada za kuonyesha hayo mambo ya ziada ambayo yamkini unaweza kuyaona kwa mwanaume mmoja usiyaone kwa mwingine. Vitu hivi vya ziada vinachochewa zaidi na nia (motive) na mwitikio (response) wa wanaume. Nia ni lengo linalomsukuma yeye kufanya vitu fulani kwa namna fulani na mwitikio ni jinsi anavyopokea mambo na mrejsho wake dhidi ya hayo. Japo vitendo na tabia zinaweza kufanana lakini unaweza kukuta nia nyuma ya kitendo na mwitikio wake dhidi ya taarifa anayoipokea ndicho hasa kinawez akumtofautisha mmoja na mwingine. Katika hili ndipo tunaweza kuona hivi vitu vya ziada ambavyo vinaweza kubeba taswira ya kumtofautisha.
Na ndio maana kwa namna fulani unaweza kuona kama anafanana na waanume wengine na kwa upande mwingine ukaona ni kama anatofautiana nao. Hivyo ukiwapima wanaume kwa vitendo na tabia zao utaona mfanano wao na ukiwapima kwa kuangalia nia na mwitikio wao utaona utofauti wao. Swali la kujiuliza ni nini chanzo cha nia nyuma ya vitendo na mwitikio dhidi ya taarifa wa mwanaume? Katika andiko hili, ninapoangazia Aina Tano za Wanaume nimejikita zaidi kwenye kuangazia kiini cha Nia na Mwitikio wao. Ukijua nia na mwitikio wa mwanaume basi ni rahisi sana kuishi na mwanaume yeyote kwa amani na furaha na hata pale inapoonekana haiwezekani uhusiano huo kuwepo basi utajua wakati sahihi na njia sahihi ya kuumaliza uhusiano huo pasipo kuhatarisha maisha yako. Tatizo kubwa linaloleta maafa kwenye jamii ni watu kutojua ukomo wa mahusiano. Wengi hujikuta wanalazimisha mahusiano yawepo ilihali yalipaswa kuwa yameisha. Ni salama zaidi ukijua pale ambapo uhusiano unapaswa kuishi. Kwa kufanya hivyo utaokoa afya yako, moyo wako na hata uhai wako. Karibu sana.
MAMBO AMBAYO HUMTENGENEZA WA MWANAUME
Unapokutana na mwanaume kwenye mazingira yoyote na kuona yupo kwa namna alivyo ni muhimu kujua kuwa hayupo hivyo kwa bahati mbaya. Hajifanyishi na wala hafanyi makusudi. Jinsi alivyo ni mjumuiko mambo mengi ambayo yametokea kwenye maisha yake ambayo wakati yanatokea pengine hata yeye hakujua madhara yake na jinsi gani yatachangia kumfanya vile alivyo. Ni watu wachache sana wanaweza kutambua kiini cha hulka na silka yake. Si jambo la kustaajabu akawa na tabia fulani ikiwa ni njema au ni mbaya na ukamuuliza kwanini yupo hivyo na akajibu tu ndivyo alivyo.
Anaposema ndivyo alivyo ni dalili tosha kuwa haoni uhusiano baina ya kile kilichowahi kutokea katika maisha yake na jinsi alivyo sasa. Asilimia kubwa ya wanaume huwa hawezi kueleza kiini cha hulka na silka zao kwa kuwa huwa aidha hawajui ama wanapuuzia athari za mambo waliyopitia kwenye maisha. Wengi hudhani wapo jinsi walivyo kwa kuwa ndivyo walivyo tu. Kuna kundi dogo ambalo huweza kutengeneza uhusiano baina ya kile kilichojiri kwenye maisha yao na vile walivyo lakini hata hivyo huwa hawa uwezo wa kuelezea kwa ufasaha hasa kwa wenzi wao. Hata hivyo ikiwa mwenzi anaweza kuwa angalau na fikra kuwa jinsi alivyo ni matokeo na historia yake basi inaweza kumrahisishia sana mwanaume huyo kuweza angalau kujielezea kwa sehemu.
Tatizo zaidi huja pale ambapo pengine anaonekana aidha anafanya makusudi na anadhamiria na dhamira yake ina nia mbaya. Katika mazingira ambayo hata yeye hajui nini hasa kimempelekea kuwa jinsi alivyo, anapojihisi kutuhumiwa na kulaumiwa kwa tabia na mwenendo wake inamuweka kwenye mazingira magumu zaidi. Katika mazingira yoyote unapokutana na mwanaume, kwa namna yoyote alivyo basi mambo haya yafuatayo ndio yamemfanya kuwa jinsi alivyo. Mambo haya huathiri namna mwanaume anavyojitazama na kujikubali na hivyo kuathiri uwezo wake wa kujiamini kama mwanaume. Huathiri uanaume wake, ile haiba ya ndani inayobeba tafsiri halisi ya jinsia yake;
1. MALEZI NA MAKUZI
Mfumo uliotumia kumlea na mazingira ambayo mtoto anakuwa yana mchango mkubwa katika kuhakikisha mwanaume anajiamini ama anapoteza hali ya kujiamini ndani yake. Kila mwanaume anaathiriwa kwa namna kubwa sana na mfumo wa malezi na mazingira aliyokulia. Alivyo inaakisi mfumo na mazingira hayo kwa kiasi kikubwa. Na mfumo na mzingira haya ndio huamua kiasi gani anafanikiwa kwenye maisha yake ya mahusiano, kitaaluma na hata kiuchumi. Mafanikio ni matokeo ya maamuzi anayofanya na kanuni anazotumia kuishi maisha yake. Akiathiriwa kwenye uwezo wake wa kuamua na kukosa kanuni zinazoongoza maisha yake ni rahisi kushindwa kwenye mambo mengi.
Wanaume wengi nyakati hizi huonekana ni waoga, wasio na msimamo, wasio na dira ya maisha na wasio na nidhamu katika maisha yao binafsi; lakini ukweli ni kuwa hii ni matokeo ya mfumo na mazingira ya malezi na makuzi yao.
2. UZOEFU WA MAISHA
Alikutana na nani? Alimuamini kiasi gani? Nini kilitokea? Hivi vyote kwa pamoja vinaweza kuathiri namna anvyojitazama. Kama alimpenda sana msichana fulani na kisha akakataliwa, ama alisalitiwa katika mahusiano, ama aliumizwa na watu aliowaamini sana; pengine alifeli katika hatua fulani ya maisha yake na akajikuta ameingia matatani na kuharibu taswira yake kwa wale waliomwamini. Wakati fulani alijihisi kusalitiwa na maisha ama na watu aliowapenda sana. Pengine alikosa msaada wa kifikra na kihisia katika hatua ambayo aliuhitaji zaidi. Ikiwa mambo ya namna hii yalimtokea katika maisha yake hasa katika kipindi ambacho hakuwa amekomaa kihisia na kifikra na akakosa msaada wa mtu aliyemwamini, inaweza kuharibu kabisa namna anavyojitazama maisha yake yote.
Uzoefu unaonyesha watoto wengi wa kiume wanaharibikiwa zaidi katika kipindi cha balehe. Hiki huwa ni kipindi kigumu zaidi cha mpito kwa mtoto wa kiume. Katika kipindi hiki huwa anafanya maamuzi mengi ambayo huweza kuletea mpasuko kifikra na kihisia. Kama akiingia matatani katika kipindi hiki na akakosa msaada wa kifikra na kihisia kutoka kwa watu anaowaamini, kuna hatari kubwa akatengeneza jeraha ambalo linaweza kudumu kwa miaka mingi ndani yake. Na pindi ambapo anathubutu kutafuta namna ya kujikwamua ndipo wengine huangukia kwenye uraibu wa vitu mbalimbali ikiwemo madawa ya kulevya, pombe, utamzamaji wa picha za ngono, kupendelea ngono na mahusiano na wanawake wengi; utazamaji filamu uliokithiri na hata uraibu wa mitandao ya kijamii na michezo ya simu (games).
Hii ni katika kupambana kujikwamua kwenye hisia za maumivu ambapo hujikuta katika uraibu mwingine ambao unaweza kumuharibia maisha yake bila yeye kujua. Hapa ni katika kuhakikisha maisha yake yanasonga mbele anajikuta amedumbukia kwenye tatizo lingine tena la kudumu. Na sasa unakutana naye katika wakati fulani na unakuta anatabia ambazo huizelewi na kwa kuwa hujui nini kiini cha tabia hizo unahisi labda ni kwa sababu ya jinsi ulivyo na pengine unajaribu kumbadilisha. Ukweli ni kwamba sio rahisi kumbadilisha kutoka kwenye kitu ambacho yeye anaamini ndicho kinamsababisha maisha yake yasogee. Ikiwa ni kubadilika basi anahitaji zaidi msaada wa kisaikolojia.
3. MAHUSIANO
Anahusiana na mwanamke wa namna gani? Mwanamke huyo ana mtazamo gani kuhusu swala la mahusiano? Kwa nyakati hizi, mahusiano imekuwa ni kiini kikubwa cha kuharibu hali ya wanaume kujiamini. Wasichojua wanawake wengi ni kuwa wanaume wengi nyakati hizi hutumia mahusiano kama nyenzo ya yeye kujiona mwanaume aliyekamili. Hata hivyo ili yeye ajione hivyo inategemea sana mwitikio wa mwanamke dhidi ya mwanaume huyo. Katika mazingira ambayo wanawake wanajiamini sana na wala hawaonekana kutilia maanani dhana hii ya uanaume wa mwanaume, wanaume wengi hupoteza mantiki ya wao kuhusiana na wanawake.
Anaanzisha mahusiano akitegemea kuwa anapata fursa ya kuonyesha uanaume wake na katikati ya safari anagundua kuwa hammudu huyu mwanamke. Suluhisho linakuwa ama ni kukatisha uhusiano huo ama kuanzisha tu mwingine hata bila ya kukatisha ule alioanzisha. Swala hapa ni kuwa hajapata alichokuwa anakitarajia hivyo anaanza kukitafuta mahali pengine. Na kwa kuwa anakuwa hana sababu za msingi ambazo anaweza kuziweka wazi kwa mpenzi wake, anajikuta ameanzisha mahusiano mengine bila kuondoka kwenye yale ya awali. Na kwa kuwa wanawake hawajui nini hasa wanaume hukitafuta inapokuja swala la mahusiano, huwa wanastaajabu nini hasa wanaume hutafuta wanaporuka kutoka uhusiano mmoja kwenda mwingine.
AINA TANO ZA WANAUME
Katika utafiti niliofanya katika kipindi cha miaka takribani kumi, nimegundua makundi haya matano ya wanaume ambayo utakutana nayo hasa kwenye tasnia ya mahusiano yao na wanawake. Makundi haya yanaweza yasijidhihirishe kwa uwazi sana hulka na silka hizi katika mahusiano ya kawaida. Ila inapokuja swala la uhusiano wa kimapenzi unaweza ukazishuhudia hulka na silka hizi kwa uwazi zaidi. Na hapa sizungumzii tabia bali mkusanyiko wa tabia kulingana na kundi husika. Mkusanyiko wa tabia fulani ndio unatengeneza kundi husika. Na hivyo katika kipindi hiki chote nimefanya utafiti na kugundua kuwa kuna mkunsanyiko wa tabia unaoshabihiana kati aina hizi. Kama nilivyosema awali kuwa kuwa jinsi walivyo ni matokeo ya malezi, uzoefu wa maisha na mahusiano waliyonayo ama waliyowahi kuwa nayo. Hili la mahusiano waliokuwa nayo linaweza kuwa kwenye kundi la uzoefu wa maisha lakini hata hivyo athari zake zinaweza kuwa na utofauti kidogo na uzoefu wa maswala mengine katika maisha. Majina haya ya makundi sio ya kitaalamu(majina rasmi) bali nimeyatoa mimi kulingana na mkusanyiko wa tabia wa kila kundi.
1. WANAUME HALISI
Hii ni aina ya wanaume ambao wamejitosheleza kifikra na kihisia. Tabia zao hazitegemei sana mwitikio wa mwanamke au mazingira aliyopo. Ni watu ambao wanajua wanachokifanya na hata akifanya jambo baya ama jema huwa ni kwa msukumo wa maamuzi na sababu binafsi tu na haina uhusiano wowote na mtu au mwenzi wake. Hili ni kundi la wanaume ambao wana dira ya maisha yao, wanajimudu kihisia na kimitazamo, wana maono ya nini wanataka kufanya kwenye maisha. Hili ni kundi ambalo kwao mahusiano/ ndoa ni kitu cha ziada ambacho anakijenga ili kimsaidie kupiga hatua moja zaidi katika kutimiza ndoto na malengo ya maisha yake. Hawaoi ama kuanzisha uhusiano kwa misingi ya upweke ama kushindwa kumudu maswala fulani binafsi ya maisha. Ni aina ya wanaume ambao mar azote huwa wanakuwa makini na swala mahusiano wanayoanzisha na ikiwa hawaoni faida wanayopata katika mahusiano husika awali watajaribu kuwekeza sana kwenye kumjenga na kumboresha mwenzi wake lakini akijiridhisha kuwa haiwezekani basi huweza kuvunja uhusiano na asiangalie nyuma. Kwa kuwa huwa wanaanzisha mahusiano kimkakati, hupenda kuwekeza sana kwenye mahusiano na inapotokea uwekezaji huo haujawa na matunda waliyodhani huwa hawaoni shida kuanza upya. Kimsingi hawa huwa na akili za kibiashara zaidi inapokuja swala mahusiano. Huangalia zaidi uhusiano huo unamnufaisha vipi katika kutimiza ndoto na malengo yake. Muhimu kwake huwa sio yeye ila malengo yake ya maisha. Hawa ni aina ya wanaume ambao hata kama ataanzisha uhusiano mwingine mbali na mwenzi wake basi uwe na uhakika kuna kitu cha thamani sana amekiona huko na lakini pia kamwe hawezi kuruhusu uhusiano alioanzisha kwingine uharibu mahusiano yake na mwenzi wake. Ni aina ya watu wenye msimamo kuhusu maamuzi yao hata kama alikosea. Hulinda sana mahusiano yao na wenzi wao na hata kama atafanya makosa atahakikisha haathiri familia yake. Hawa ni aina ya wanaume ambao wapo tayari kubeba lawama ikiwa tu kwa kufanya hivyo atalinda kile anachokithamini. Akiamua kuoa basi kamwe hawezi kuruhusu mtu yeyote aingie katikati yake yeye na familia yake. Iwe ni ndugu, mzazi au rafiki. Hupenda kutenganisha mahusiano yao na watu wengine na familia zao. Uanaume wao hupenda kuuonyesha kwa kutimiza majukumu yao ya msingi ya kifamilia. Hata kama atakuwa na mapungufu mengi lakini atahakikisha anatimiza wajibu wake kama mume na baba kwa namna yoyote ile. Kamwe hawezi kujitetea inapokuja swala la kutimiza wajibu wake wa msingi. Changamoto ya kundi hili ni kuwa kuna lina uwezekano wa kudumbukia kwenye kundi la “wanaume sungura”. Idadi kubwa ya wanaume sungura hutokana na kundi hili.
2. WANAUME SUNGURA
Hili ni kundi ambalo wanaume tabia zao huchochewa zaidi na hulka na silka ya aina ya mwanamke aliye naye. Nasema “kuchochewa” sio kuanzishwa. Hapa sikusudii kumlaumu mwanamke mwenye hulka na silka ya namna fulani lakini tu ni muhimu kujua kuwa kundi hili ni la aina ya wanaume ambao kwa asili na kawaida huwa wanajimudu, wanajielewa na wanajua wanachofanya na hivyo kuchipuka kwa tabia hii lazima kunachochewa na kitu nje sio ndani yake. Ikiwa mwanaume halisi atakuwa na mwanamke amabaye atajihisi kuwa anashindwa kummudu kuna hatari akadumbukia kwenye kundi hili. Kama nilivyosema awali, kundi la wanaume halisi huwa hawapendi kutengeneza sintofahamu kwasababu ya maamuzi ambayo waliyafanya wenyewe. Hivyo badala ya kupambana na mwanamke, kundi hili hujifanya kama “wameshindwa vita” ila wanatengeneza agenda za siri. Nawaita wanaume “sungura sungura”. Akiwa mbele ya mwenzi wake anakuwa mpole, mwema, mwaminifu na mstaarabu. Hata mwanamke akimgombeza, akimtukana, akimdhalilisha, akimdharau, akimkosoa; yeye hatokimbilia kwenye kugombana ama kubishana. Ni kama ameshindwa vita. Hapambani, hajibu, habishani, hapigi, halazimishi jambo. Hawa hautawakuta amepiga au kumdhalilisha mke wake. Tatizo la kundi hili ni kuwa wanaamua kutengeneza mfumo mwingine wa maisha nje ya mahusiano yao ili maisha yaendelee. Inaweza kuwa mahusiano na mwanamke/wanawake wengine ambao wanaona kuwa wanawapa heshima yao kama wanaume na wanaweza kutimiza matarajio na malengo yao ama shughuli zingine zozote zitakazomfanya awe huru kuonyesha uanaume wake huko. Mahusiano hayo yanaweza kuwa yakimapenzi ama sio ya kimapenzi ila kivyovyote vile uwe na uhakika ikiwa ataanzisha basi anajua haswa nini anakitafuta. Sio watu ambao husukumwa zaidi na hisia kiasi cha kuanzisha mahusiano kwa bahati mbaya. Na hata ikitokea akianzisha uhusiano kwa bahati mbaya basi aidha atautengenezea lengo au hautadumu kwa muda mrefu. Pamoja na yote hayo bado atajitahidi kuilinda sana ndoa na familia yake na hivyo hawa ni aina ya wanaume ambayo kujua kuwa anauhusiano mwingine ni lazima ufanye uchunguzi wa kina. Huwa hawatarajii kuwa mwenzi wake atajua kile anachofanya na ndio dhana ya “usungura” inapokuja. Hatoacha kuhudumia familia na kutimiza wajibu wake kama mume na kama baba. Kama ilivyo kwa wanaume halisi, hawa hujitahidi kutochanganya mambo yao binafsi na maswala ya familia yake.
Kama mwanamke anakuwa na nguvu kubwa dhidi ya mwenzi wake na mume haonekani kuwa na tatizo na hali hiyo ni vizuri kuchukua tahadhari. Kuna uwezekano mkubwa mwanaume kukuacha wewe ujione kuwa unaweza kumfanya chochote na kisha akatoa nafasi kwa mtu mwingine ambaye anaweza kuharibu zaidi mahusiano yenu. Kwa asili mwanaume katika uanaume wake hawezi kukubali kutawaliwa kirahisi. Kama ameruhusu hilo ni muhimu kuwa makini. Hisia hasi zisizozungumzwa ambazo zipo ndani ya mwanaume ni hatari sana kwani zaweza kumpelekea kufanya vitendo vya siri ambavyo vinaweza kuweka maisha yake na mwenzi wake hatarini. Ijapokuwa ni kundi ambalo hujitahidi sana kulinda familia yake lakini si mara zote anaweza kufanikiwa na hivyo kuna haja ya kufunga milango inayoweza kuchochea tabia hii ndani yake.
Kumbuka kuwa kundi hili ni la wanaume ambao hawaonagi fahari kutokuwa waaminifu kwa wenzi wao. Swala la kutokuwa waaminifu kwao ni matokeo ya kile kinachotokea ndani ya mahusiano yake. Ikiwa mahusiano baina yake na mwenzi wake wake yataboreshwa basi uwezekano wa yeye kubadili mfumo mzima wa maisha yake ni mkubwa. Kimsingi hawa ni kundi la wanaume ambao ni rahisi zaidi kuwabadilisha tabia zao maana walivyo huwa ni matokeo ya vile mwanamke wake alivyo. Hivyo mwanamke akibadilika ni rahisi yeye pia kubadilika. Changamoto hapa ni kuwa hawawezi kukwambia kuwa nafanya hivi kwa sababu ya vile ulivyo. Kwa kuwa hatopenda kumuumiza mwenzi wake kitu chepesi kwake kinakuwa ni kujitengenezea mfumo mwingine wa maisha pembeni ambao kwa vile anahisi mwenzi wake hatojua inamfanya aamini kuwa hawezi kumuumiza. Shida inaanza pale ambapo mwenzi wake anajua siri zake kinyume cha matarajio yake ndipo anajikuta kwenye wakati mgumu. Unaposikia wanawake wanafundishwa na kufundwa basi wengi huwa wanataswira ya wanaume wa kwenye kundi hili ambao tunaamini kuwa mke akiwa bora basi mume atakuwa bora pia lakini ukweli na uhalisi wa mambo ni kwamba kuna makundi mengine ya wanaume ambao hata kama mke awe bora kwa kiasi gani bado atakutana na changamoto tu namna ya kuishi nayo.
3. WANAUME WADHALILISHAJI
Hili ni kundi ambapo wanaume wanaamua kutumia nguvu kutetea uanaume wao. Hawakubali kuonekana wameshindwa. Wanadhihirisha hisia zao za kuhisi kuvunjiwa heshima wazi wazi kwa kukabiliana uso kwa uso. Ijapokuwa tafsiri ya kuvunjiwa heshima inaweza kutofautiana baina ya mmoja na mwingine, kinachowaleta pamoja wanaume wa kundi hili ni namna wanavyoitikia(respond) pale anapohisi kuwa nafasi yake ya uanaume inatishiwa. Kama nilivyotangulia kusema awali hali hii inawezekana ikasababishwa na malezi, makuzi, uzoefu au aina ya mahusiano aliyonayo. Hivyo sio kila wakati inaweza kuwa tabia hii inachochewa na mwenzi wake bali ni matokeo ya mambo yaliyotokea huko nyuma.
Kuna wanaume wa kwenye kundi hili ambao wapo tu hivyo walivyo bila kujali aina ya mwenzi aliyenaye na kuna wale ambao wapo hivi kwasababu ya aina ya mwenzi aliyenaye. Kinacholifanya kundi hili liwepo na namna hii ya mwitikio wao wa kupambana na wenzi wao. Hili ni kundi la wanaume ambao wanaweza kumpinga mwenzi wake hata katika mambo ya msingi na yenye faida. Anaweza asichukue ushauri mzuri wa mwezi wake japokuwa anajua kuwa faida zake kwa hofu kuwa atatawaliwa. Atapenda atawale kila kitu kwa msingi wa mawazo yake hata kama atakosea ili kuthibitisha tu kuwa yeye ni mwanaume. Kwake yeye, mwanamke hana nafasi ya kumwambia nini cha kufanya si kwa sababu mwanamke hana uwezo huo bali anaona kama atadhalaulika kwa kumpa nafasi hiyo mwanamke. Hapa ni swala la hofu zaidi ndio linalomwongoza walakini hofu hiyo anaidhihirisha kwa kuwa mbabe na mbishi. Anahofia usalama wa nafasi yake kama mwanaume ndani ya mahusiano na hivyo anaipigania. Hii wakati mwingine inaweza kupelekea mwanamke akajihisi kuwa pengine hana uwezo wa kumshauri lakini si kweli. Uwezo anaweza kuwa nao na hata mwanaume anajua hilo ila hana uhakika na matokeo ya kuupokea huo ushauri hivyo anajitengenezea wigo wa kutopokea ushauri huo. Akifanikiwa awe ni yeye na akifeli basi awe ni yeye. Udhalilishaji wa kingono, kihisi, kimwili na kijinsia unazidi kushamiri katika jamii nje na ndani ya ndoa. Tunashuhudia matukio ya hatari sana katika jamii yakifanywa na wanaume. Ubakaji, udhalilishaji, unyanyasaji, kuingilia wanawake kinyume na maumbile; rushwa za ngono, mabosi kulala na wafanyakazi wao kwa lazima, walimu kulala na wanafunzi wao.
Vitendo hivi huchukuliwa kama ni tamaa za wanaume na mfumo dume tu lakini kuna tatizo kubwa zaidi ya hilo. Wanaume wamepoteza hali ya kujikubali na sasa wanatumia misuli, ushawishi na nafasi zao kama silaha ya kutetea heshima yao wanayohisi imepotea. Wakati mwanaume sungura anaitafuta heshima nje ya mwenzi wake na anajitahidi kuficha, kundi hili huamua kupambana uso kwa uso na mwanamke anayeonyesha kumvunjia heshima yake hata kama ni mkewe. Na huu unakuwa ndio mwanzo wa udhalilishaji kwa kuwa hapa anakuwa kama anapimana naye ubavu na kumdhibitishia kuwa yeye ni mwanaume na mwanamke hawezi kumshushia hadhi na heshima yake. Hapa ni mwanaume aliyepoteza hali ya kujiamini na kujikubali na hivyo ile busara na hekima ya kumuheshimu mwanamke inaondoka. Atataka kutumia kila njia kuthibitisha kuwa yeye ni mwanaume kamili.
Mwanaume aliyepoteza hali ya kujiamini na kujikubalihawezi kuwa na busara na hekima ya kumuheshimumwanamke
Wanawake kwenye jamii na hata katika ndoa wamejikuta katika mazingira magumu. Wanajaribu kufanya kila wanachoweza kutimiza kile kinachodhaniwa kutofurahia na kutoridhishwa kwa wanaume lakini mwisho wa yote wanaishia kuumizwa zaidi. Wanajaribu kuwa wabunifu wa mambo na kutafuta hekima ya namna ya kuishi na kuhudumia mwanaume. Wanawake wanachofanya ni kutibu “dalili za ugonjwa” na sio “ugonjwa wenyewe”. Ugonjwa halisi ni wanaume kupoteza kujiamini hivyo kila wanachotaka ni kwa ajili ya kutafuta kutibu mashaka yao. Na hicho wanachofanya na wanawake sio tiba ya tatizo halisi.
Tatizo kubwa hapa kwa kundi hili la wanaume ni usalama wa nafasi yao kama wanaume. Wanakuwa hivyo kwa kuwa wanahisi kuvunjiwa heshima na Mwanaume aliyepoteza hali ya kujiamini na kujikubali hawezi kuwa na busara na hekima ya kumuheshimu mwanamke nafasi zao kama wanaume kuporwa. Ile nafasi ya kutawala na kuongoza, ya kufanya maamuzi bila kupingwa au kukosolewa, nafasi ya kuaminika kama kiongozi wa mahusiano na familia. Hivyo basi ukiacha mambo mengine mengi ambayo uanweza kujaribu kumfanyia basi haya mawili ni muhimu zaidi;
- Elewa tafsiri yake ya kuheshimiwa.
- Muhakikishie usalama wa nafasi yake kama mwanaume haijalishi uwezo wake katika kuongoza mahusiano, familia na hata maisha.
Haya mawili yanatosha sana kumfanya mwanaume wa kwenye kundi hili kuondokana na nia ya kupingana na kushindana na mwenzi wake. Anachohitaji ni uhakika tu kuwa yeye ndio mume, kiongozi, mtawala. Yeye ndio amebeba dira na hatima ya kule mnapoelekea. Sasa inawezekana ukawa huamini uwezo wake lakini kuendelea kutoamini kunaweza kuwa na madhara ambayo nimeyaeleza hapo juu. Hivyo ni vema ukajenga imani ili upate nafasi ya kuaminika kiasi cha kutosha kuweza kushauri. Maana asipokuamini hawezi kukupa nafasi ya kushauri na usipokuwa na nafasi mambo yataharibika na hutakuwa na cha kufanya.
Ukweli ni kuwa kundi hili ni wanaume ambao wakati mwingine wanaelewa kuwa mwenzi wake anayo hekima na busara ya kutosha kumshauri isipokuwa hofu ya kutawaliwa ndiyo hufanya wasionyeshe kuwaamini wenzi wao. Hivyo kumuhakikishia usalama wa nafasi yake kama mume kuna faida kubwa kwenu nyote.
4. WANAUME WALIOKATIA TAMAA UANAUME WAO
Hili ni kundi la wale ambao wamekata tamaa kupambania uanaume wao. Maisha yamewavuruga, dira imepotea, uelekeo hawauoni, ulimwengu umewasaliti, waliowaamini waliwaumiza, umri umeenda, wamepishana na wakati, fursa zimewapita, wamepoteza tumaini; na hivyo nia na hamasa ya kupambana imekufa na sasa wanaishi maisha yao kwa kusogeza siku. Hapa ndipo unakutana na wanaume ambao hawana malengo ya maisha, hawana bidii ya kazi, wavivu, walevi, wanaweza kulala na mwanamke yoyote popote(bila kujali umri, hadhi wala mazingira), kazi hawana na wala hawatafuti, na hata kama ana kazi wala haijali. Kifupi hajali kinachoendelea kwenye maisha wala hajijali yeye mwenyewe; hapa utakutana na wale wanaume ambao nao wanataka kulelewa na kuhudumiwa(ikiwa na wanawake ama wanaume wenzao) na hawaoni shida na katika kundi hili ndimo pia kuna mashoga. Kwa wengi hizi huonekana kama ni tabia ambayo mtu amejijengea lakini ukweli ni kwamba wengi wao ni matokeo ya malezi, mazingira waliokulia ama uzoefu wa maisha au muunganiko wa vyote vitatu.
Njiani walipoteza kujiona na kujikubali kuwa wao ni wanaume. Walijaribu kupambana lakini mazingira hayakuwaruhusu. Walishindwa kusimamia asili yao wakajikuta wameangukia upande mwingine. Kwa wengi hali hii huanzia wakiwa wadogo na huendelea kukomaa katika fikra na mtazamo wao. Hali ya kuona kuwa dunia haiwajali. Kuona kuwa ulimwengu hauwathamini na inawaonea. Kadiri wanavyozidi kupambana na kukutana na mambo ya kuwavunja moyo ndivyo wanazidi kukata tamaa. Tabia hizo ni matokeo ya uharibifu ambao umekwisha kutokea ndani yao. Wengi huanza kwa kujificha, kwa aibu, kwa kujitenga na kisha kadri wanavyoendelea wanafanikiwa kuishinda ile aibu na kujiweka wazi. Wanaikubali ile hali na kuanza kuwachukia wale wanaopingana nao hata kama ni wenzi wao. Kule kuona aibu na kujificha ni ishara tosha kuwa wanajua wanachofanya sio sahihi na wengi hutamani wasifanye hivyo bali kule kupoteza kujiamini ndiko huwapelekea kuangukia kwenye mtego huo. Unapotaka kumsaidia kitu cha msingi zaidi cha kumjengea ni hiyo hali ya kujiamini na kujikubali kuwa yeye ni mwanaume. Vile vitendo anavyofanya sio tatizo kubwa kuliko kile kinachoendelea ndani yake. Kwa kuwa kiini cha tatizo lao ni kuhisi kukataliwa, hupenda wakubalike mawazo na tabia zao hata kama ni mbaya na za aibu.
Kila anayeonyesha kumpinga anakuwa adui yake kwa kuwa anatonesha kidonda chake. Ukitaka kuwa rafiki yake basi muunge mkono mambo anayofanya hata kama ni ya fedheha. Anaweza kuwa ni mlevi, mvivu, muhuni, asijejali kazi, hana dira ya maisha, hana mipango na malengo yoyote, tabia zake hazieleweki, nyumbani anapotea hata siku kadhaa; lakini kitendo cha kumkosoa na kumuonyesha kuwa anachofanya sio sahihi unakuwa unaongeza tatizo. Hatua aliyofikia inakuwa ni hatua yay eye kutojali nani anasema nini. Unaweza kumpeleka kwenye vikao vya ndugu, wazazi na viongozi. Hawa ni kundi la wanaume ambao wamefika hatua haogopi mtu yoyote hata kama ana mamlaka juu yake. Hatishwi na mzazi wala bosi wake. Hivyo kumpeleka kumshitaki huko haiwezi kuleta suluhisho. Kumbuka kuwa huyu ni mtu ambaye ameshakata tama hivyo hana cha kupoteza. Namna nzuri ya kumsaidia ni kuwa rafiki yake ambaye anaweza kukuamini. Kundi hili ni aina ambayo inahitaji msaada wa kisaikolojia ili kuweza kusaidiwa kwa kuwa ni ngumu sana watu wake wa karibu kuweza kumsaidia maana atahisi kama wanamuhukumu. Hata hivyo ili aweze kumwamini mtaalamu wa kumshauri anahitaji angalau kupata uungwaji mkono wa mtu anayemuamini. Hivyo kama una rafiki au mwenzi ambaye amefikia hatua hii kitu muhimu cha kwanza ni kuhakikisha unakuwa na uhusiano mzuri nay eye kiasi cha yeye kukuamini na kisha unaweza kumshauri aweze kupata usaidizi wa kisaikolojia. Muhimu ni kuhakikisha kuwa hajisikii kushutumiwa au kulaumiwa kwa jinsi alivyo.
5. WANAUME HATARI
Hili ndio kundi pekee la wanaume ambao wanaweza kuua ama kujeruhi vibaya wenzi wao. Tunapozungumzia ukatili wa kimwili basi uanhusishwa zaidi na kundi hili. Kwa wengi hudhani kuwa wivu wa mapenzi. Mara nyingi tunaposikia mwanaume ameua mke ama mpenzi wake, maelezo huwa ni wivu wa mapenzi ila sio kweli. Kila mwanaume huwa na wivu wa kimapenzi kwa mwanamke anayempenda ila sio kila mwanaume anaweza kufika hatua ya kupiga, kumjeruhi na kumuua mwenzi wake kwa kigezo cha wivu. Wivu pekee hautoshi kuua mtu. Hawa ni watu ambao huwa wana tatizo la kiakili. Tatizo hili hutokana na matukio fulani kwenye maisha yake ambayo yalimuumiza sana kiasi kwamba anakuwa na chuki iliyopitiliza kwa mtu yoyote ambaye humuumiza ama kuonyesha dalili za kumuumiza. Anakuwa na jeraha kubwa ndani yake na pindi ukilitonesha akili yake inaruka na kujikuta amefanya tukio ambalo hakutegemea kulifanya.
Kundi hili hutokana watoto wanaofanyiwa matukio ya kuumiza wakiwa kwenye umri na mazingira ambayo hawawezi kujitetea, mathalani anateswa na kudhalilishwa na kisha anatishwa asiseme au hata akisema haaminiki na hakuna anayejali, ama pengine anahofu kuwa akisema inaweza kumletea aibu au ikaleta madhara mabaya kwenye jamii husika. Kundi hili la watoto mara nyingi hukuwa na majeraha ndani. Majeraha haya kwa kuwa hayapati nafasi ya kupona hukuwa nayo na wakati fulani huonekana kana kwamba wapo sawa lakini bado ndani wanakuwa wagonjwa. Kinachotokea kwa wakati wanafanyiwa matukio hayo bila kuwa na msaada, wengi huamini kuwa wanafanyiwa hivyo kwa kuwa hawana uwezo wa kujitetea na hivyo huwa wanajiapiza kuwa nikiwa mkubwa au nikipata uwezo wa kujitetea kamwe sitomruhusu mtu anaifanyie kitu kitakachoniumiza.
Haya huwa wanakuwa wakitafuta namna ya kupambana na kila mtu ambaye atajaribu kumuumiza. Hivyo bidii yao ya kwenye maisha huwa inachochewa na uchungu na shauku ya wao kupata uwezo wa kujitetea. Huwa wanakuwa wakiwa na jeraha ndani ambalo kamwe hatotaka mtu aliguse na pindi anapohisi mtu anaeleke kumuumiza yeye huwahi na kumuumiza mtu yule. Kwa ujumla hawa ni watu ambao huwa hawzwezi kustahimili kuumizwa na huona ni heri wao kuumiza wengine kuliko kuumizwa wao. Hii kupenda kujihami zaidi na kuwahi kuumiza wengine ndio hupelekea wao kufanya matukio ya hatari. Aina hii ya wanaume huwa wana haiba mbili. Kwa nje kama humfahamu huwa ni watu wanaoonekana watulivu, wema, wastaarabu na wapole sana na ni rahisi sana kukushawishi kuwa yeye ni mtu sahihi ila ndani yao huwa wana haiba ya ukatili ulipotiliza. Japokuwa hali hii huwa pia inakuwepo kwa wanawake ila kwa wanaume huwa inajidhihirisha kwa haraka zaidi. Majeraha haya sugu hupelekea tatizo la kiakili (mental disorder) na mara nyingi tatizo hili hujidhirisha kama wivu wa kimapenzi.
0 Comments