NEW

6/recent/ticker-posts

Advertisement

Unahitaji kuwa mpelelezi na unaipenda hii kazi?





“..je, ni mali? Ufahari? Mshawasha au Uzalendo? Kwa nini wataka kuwa ‘spy’…”


Kuna siku fulani kuna mzee niliwahi kumsikia akiongea maneno fulani akimwambia mtu mwingine, maneno ambayo hayajawahi kutoka kichwani mwangu kwa miaka kadhaa sasa.
Yule mzee alisema..
“kwenye hii kazi, karibia nusu ya muda wako wote kazini hautojua sababu kwa nini unatumwa kufanya hicho unachokifanya.!”
Nayakumbuka sana haya maneno kwa sababu yana ukweli mkubwa sana ndani yake.
 
Inawezekana kila mmoja humu kuna kijana unamfahamu ambaye unajua anatamani kuwa mwajiriwa kwenye idara za intelijensia. Au pengine hata wewe mwenyewe umewahi kutamani. Pia binafsi mara kadhaa nakutana na vijana wa namna hii, anakwambia 
“..Bro natamani kuwa ‘kipepeo’..”
Mara zote swali la kwanza ambalo huwa nawauliza ni kwa nini? kwa nini utake ajira ya dizaini hyo? Kwa nini hautamani kuwa daktari, mwalimu. Mwanasheria, afisa wa benki? Kwa nini utake kazi ya sampuli hii?
Mara nyingi watakujibu kwamba
 “..naipenda hii kazi tangu nikiwa mdogo.” 
Hili si jawabu sababu bado swali linabaki pale pale… kwa nini uipende kazi hii na si nyingine?
 
Ukifanya tathimini watu walioko kwenye hizo idara na wale ambao wanatamani kuingia wanaangukia kwenye makundi manne kwa nini wako kwenye hizo idara au kwa nini wanatamani kuingia huko.
 
Kundi la kwanza, ni la watu ambao wameingia kwenye idara hizo (au wanatamani kuingia) sababu ya ‘Ufahari’. Wanahisi kwamba akiwa afisa wa idara ya intelijensia basi anakuwa ni mtu wa daraja fulani tofauti na raia wengine. Anahisi kazi hiyo inamtofautisha na kumfanya binadamu wa tofauti. Anatamani ile hofu, heshima na mshangao watu wanaokuwa nao wakimuona ‘afisa usalama’.
 
Kundi la pili ni la watu ambao wameingia kwenye idara zetu hizi (au wanatamani kuingia) sababu ya kupata ‘thrill’ (nakosa neo zuri la lugha yetu hivyo nitatumia mshawasha’). Watu hawa wanaona kwenye sinema, au wanasikia hadithi kwa watu na wanajikuta wanatamani yale maisha ya kukimbizana kusaka wahalifu, maisha ya kusaka siri za adui, maisha ya kuficha siri, maisha ya kuishi ‘gizani’, maisha ya vitendawili na kutegua mafumbo, maisha ya mchaka mchaka. Anatamani kuishi kwenye hiyo ‘thrill’ ya maisha ya namna hiyo.
 
Kundi la tatu ni la watu ambao wameingia kwenye hizi idara (au wanatamani kuingia) sababu ya kuchuma utajiri. Wako ambao wanatamani mishahara minono na marupurupu ambayo wanasikia maafisa usalama wanalipwa. Wako ambao wanaamini wakiingia kwenye sekta hiyo itakuwa rahisi kwake kufanya biashara fulani ikafanikiwa kwa wepesi kutokana na ‘connection’ ambazo atazipata huko.
 
Lakini liko kundi la tatu, ambalo wako wachache mno ambao wameingia kwenye sekta hii kwa sababu ya uchungu walionao mioyoni kwa sababu ya nchi yao. Anajua matishio ambayo nchi iko nayo na anatamani awe sehemu ya kuyakabili. Anajua kwamba amani ya nchi ni tunu adhimu na anataka awe sehemu ya kuidumisha. Anajua ulazima wa kafara ya nafsi yake ambayo anatakiwa kuifanya ili kutimiza malengo hayo. Anajua ni kiasi gani nchi yake inamuhitaji.
Hawa ni wachache mno. Hata uko kwenye hizi idra, wako wachache sana japo kila aliyepo huko na hata wale wanaotamani kuingia huko watataka kukuaminisha kwamba wako kwenye kundi hili la nne.
 
Ubaya ni kwamba ni ngumu kujiridhisha dhamira ya mtu kwa asilimia mia moja sababu moyo wa mtu ni giza totoro ambalo huwezi kuona hata kwa tochi. Hakuna idara ambayo inaweza kufanya ‘vetting’ kujua dhamira ya mtu kwa asilimia mia moja. Kuna procedures, guidelines, techniques na principles ambazo zinatumika kum-recreuit afisa mpya, lakini bado huwezi kuijua dhamira yake kwa asilimia mia moja. Ndio maana bado wako maafisa kwenye kila idara ya ujasusi duniani wanaogeuka wasaliti, wako wanao kula rushwa, wako wanaodhuru watu kwa sababu ya uafisa wao, wako wanaotumia huo mgongo kuchuma mali. Ni kwamba hawakuwa vetted? Hapana, walifanyiwa vetting, lakini hakuna vetting inayoweza kukuonyesha nafsi ya mtu na dhamira yake.

Ndio maana kila nikimsikia kijana anasema anatamani kuwa ‘kipepeo’ nitamuuliza 
“Kwa nini.. kwa nini unaitaka kazi hiyo na si nyingine?”
na karibia 97% watakupa jibu ambalo si sahihi (naipenda sana hii kazi tangu nikiwa mdogo).
Suala hili la watu kuingia kwenye hizi idara wakiwa na sababu ambazo si sahihi ni moja ya changamoto kubwa ambayo kila idara inawakabili sababu huko mbeleni watu hawa wanakuja kugeuka mwiba… pengine wanakuwa mwiba sababu ya ufanisi mdogo wa utendaji kazi na mara nyingine kadhaa watu hawa wanaweza kugeuka kuwa maadui wa idara kabisa kwa namna tofauti.

Post a Comment

0 Comments