NEW

6/recent/ticker-posts

Advertisement

Yawezekana tulikuwa na Bunge bila Spika. Tunakoelekea tunaweza kuwa na Spika bila bunge. Bila ushabiki wala uzembe, tuangalie yafuatayo kwa makini:


MAMA TUVUSHE, TUKUVUSHE

By Askofu Bagonza, PhD


1. Ukubwa wa CCM si mtaji, ni hatari. Bila upinzani imara, CCM ni sawa na chatu aliyefugwa ndani chungu cha mfinyanzi. Akikosa chakula atamla mfugaji.

2. Mihimili mitatu ya kufikirika ni hatari kwa nchi. Mmoja juu ya mingine ni kitanzi cha amani yetu.Tatizo si anayefunika. Wanaofunikwa wanapenda.

3. Isiwe sheria wakuu wa mihimili kualikana kila wakati na kila mahali. Tunadhoofisha uadilifu wa mihimili yote. Kujipendekeza kumestawishwa kupitia huko.

4. Tuharamishe kujipendekeza kama tulivyoharamisha kukashifu Viongozi.

5. Mgombea binafsi anaweza kuwa Spika mzuri ili kuokoa uadilifu wa bunge.  Kama mahakama isivyo na mahakimu/majaji wenye vyama na Spika asiwe na chama.

6. Afya ya Taifa ni mshikamano wa dini mbalimbali, makabila, jinsia, na itikadi mbalimbali. Mshindi anayechukua vyote ni sumu kwa amani yetu. Bora upinzani wa nje kuliko wa ndani.

7. Mjadala wa Haja ya kuwa na Katiba Mpya usitishwe. Huu ni wakati wa kutekeleza si kujadili. Wasioidai inawafaa kuliko wanaoidai.

8. Tangu uhuru tumetawaliwa na chama kimoja awamu tofauti. Kila awamu ina mambo yake. Zipo zilizotawanya na kurarua. Namlilia Mungu ili hii ya (6 au ya 5) iwe ya kuunganisha na kuponya majeraha. Anayesita zamu yake yaja.

9. Sakata la Ndugai (Ndugaigate) limefunua aibu yetu. Mfumo dume uko imara lakini pia bibi mwenye ndizi mbivu hakosi wajukuu wa kutuma mtoni. Waliojituma hongera, mliotumwa kuna siku mtatumwa kutafuta vitanzi vyenu.

10. MUNGU YUPO na ANATUONA. Si kila kitu tulichofanya 2020 kilibarikiwa na Mungu! Tukubali aturekebishe kwa sababu tumemtaja sana tangu 2020 na tumeshika misahafu tukaapa kwa jina lake. ZINGATIA HILI: Pasipo na haki huwa hayupo.

MAMA TUVUSHE ILI TUKUVUSHE. Kama una mashaka, Kuna MWAMBA mzoefu wa kuvusha, anaweza kusaidia.

Mama historia umeiweka. Bado Legacy.

Post a Comment

0 Comments