Idadi ya Wamasai inaongezeka, sawa je idadi ya Nyumbu na wanyama wengine haiongezeki? Ama ingewezekanaje hao wamasai wasiongezeke? Wao sio binadamu kiasi kwamba wakose haki ya kuzaliana?
Eneo la hifadhi ya Ngorongoro ni zao la mkataba kati ya Serikali ya kikoloni ya Uingereza na viongozi wa kimila wa jamii ya kimasai na makubaliano yalikuwa ni kwamba,wananchi wenyeji wa Ngorongoro waondoke eneo la Serengeti na wasirudi tena waende Ngorongoro
Mkataba wa Serikali ya kikoloni ya Uingereza na viongozi wa kimila uliainisha kuwa,wananchi walioamua kutoka Serengeti, wananchi hao hawataondolewa tena katika maeneo waliyohamia (Ngorongoro) na wataendeleza maeneo hayo na pia huduma za kijamii zitatolewa.
Eneo la mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro likaundiwa sheria yake, eneo la Loliondo likaendelea kusimamiwa na Sheria ya wanyamapori ya wakati ule ya mwaka 1951 na sasa sheria ya wanyama pori ya Tanzania ya mwaka 1974.
Sheria ya wanyamapori ya mwaka a 1974 imeainisha aina kuu tatu za hifadhi
1. Hifadhi za Taifa
2. Game reserve
3. Game control area (maeneo ya wanyama lakini ni ya wananchi), kuna upotoshaji kuwa wananchi wa Loliondo wameingilia kitalu cha uwindaji,
Kuna propaganda zinaendelea kwamba mifugo imeongezeka na shughuli za kibinadamu zimeongezeka nakuna uharibifu wa mazingira.
Kuna idadi ya Nyumbu milioni 1.7, idadi ya Ng'ombe kwa upande wa Loliondo 235000, na ukichanganya na wanyama wengine wanakuwa 400,000., unaweza kuona Ng'ombe ni wachache kuliko wanyama pori wengine.
Propaganda nyingine ni kuwa wenyeji wamezidi wamefikia 184, 000, watalii wanaoingia ni 700,000 , kati ya watalii 700,000 na wenyeji 184, 000 ni wepi ni wengi na wapi ambao wataharibu mazingira?
Propaganda nyingine wanasema idadi ya Wamasai inaongezeka,sawa je idadi ya Nyumbu na wanyama wengine haiongezeki? Ama ingewezekanaje hao wamasai wasiongezeke? Wao sio binadamu kiasi kwamba wakose haki ya kuzaliana?
Kwenye baadhi ya vyombo vya habari na waandishi maslahi binafsi vimeeleza kuwa, Ngorongoro baada ya mitatu itatoweka, kwanini itoweke wakati ilikuwepo kwa miaka mingi iliyopita?
Tatizo la Wamasai katika hifadhi ya Ngorongoro ilianza rasmi mwaka 1992 na kujulikana kama Kashfa ya Loliondo,ambapo serikali ikatoa eneo la Loliondo (game controlled area) kwa kampuni ya OBC na mgogoro huu umeanza baada ya mwekezaji kuingia katika eneo hilo.
Hatuamini kama mgogoro wa Ngorongoro utaisha kwa kutumia vyombo vya habari na waandishi kutengeneza propaganda zisizo kweli, bali utaisha kwa kuwashirikisha wananchi, kuna sheria, mikataba,haki za binadamu, heshima kesi iliyokuwepo mahakamani katika mahakama ya Afrika Mashariki.
Tunaamini uongozi wa juu wa serikali hauna taarifa za mgogoro huu na wananchi wanadanganywa kuhusu mgogoro huu kwamba Wamasai wanatakiwa waondoke hapo, na wanaotengeneza propaganda za kuonyesha kuwa wamasai wanaharibu hifadhi kimsingi ndio wanapaswa kuwalinda.
Mwaka 2009 mgogoro huu ulifika kwenye kilele chake na taarifa zake zipo na kuliripotiwa ukiukwaji wa haki za binadamu,watu walipigwa, walichomewa maboma, walitobolewa macho,kwa nini tutumie mabavu na si kuwashirikisha wananchi?
Kwanini kunakuwepo mitizamo tofauti kwa viongozi wa serikali kuhusu mgogoro huu? mara waondoke, mara ardhi ya kijiji, mara ardhi ya hifadhi. Kwanini tusitafute tafsiri ya kisheria bila kutisha, kukamata mtu, bila kutumia nguvu?
Shida ya Ngorongoro inatokana na ushirikishwaji hafifu wa wananchi, wahifadhi hawataki wanatumia propaganda za magazeti na wanahabari maslahi binafsi kuaminisha umma na serikali kwamba Wamasai ni waharibifu wa mazingira na wanapaswa kuondoka.
Hakuna mazingira yoyote yaliyowekwa kwa wahifadhi kukutana na kumzungumza na wananchi kuhusu mustakabali wa Ngorongoro zaidi ya vitisho na matumizi ya nguvu.
Mwaka 2017 kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na kupelekea wananchi kupitia vijiji vyao kwenda Mahakama ya Afrika Mashariki wakilalamika kwamba mgogoro huo na mambo wanayofanyiwa yanakiuka haki za binadamu na sheria ya ardhi ya mwaka 1999 na kesi inaendelea
Wahifadhi wa hifadhi ya Ngorongoro hawawezi kutoka hadharani kusema haya maneno ya kuwadhalilisha wamasai,Kwa sababu sheria inawataka wahifadhi walinde wanyama na wamasai, ndio maana wameajiri vyombo vya habari kufanya propaganda ya kuwadhalilisha wamasai
Mwaka juzi kulikuwa na nia ya serikali ya kuwaondoa wananchi wa Loliondo, wakakimbilia mahakamani, mahakama ilitoa amri ya kusitisha kuwaondoa hadi kesi itakapoisha,lakini Mkuu wa Mkoa wa Arusha akaenda Loliondo na kuwaambia kuwa wananchi wataondolewa,je huu ni utawala wa sheria?
Wajibu wa vyombo vya habari na wanahabari makini ni kusimama na jamii, ikitokea Mwandishi wa habari anakwambia wamasai wanaharibu Ngorongoro na wanatakiwa waondolewe basi nyuma yake kuna malipo haramu amepata ili kutweza utu wa wamasai kwani wako kisheria
Tunatumia ukurasa huu kumpa elimu ya bure Maulid Kitenge kuwa wamasai walioko ndani ya hifadhi ya Ngorongoro wako kwa muujibu wa sheria na mamlaka ya hifadhi inapaswa kuwalinda ndio maana haitoki hadharani kusema haya anayosema yeye.
0 Comments